Narok, Februari 24,2026 KNA Na Emily Kadzo

Daraja la Mogor laporomoka kufuatia mvua mkubwa eneo la Kilgoris

Wakaazi wa Kilgoris katika Kaunti ya Narok wanaiomba serikali ya Kaunti na ile ya Kitaifa kulijenga daraja la Mogor kwa upesi kufuatia kuporomoka kwake hii leo baada ya mto Mogor kuvunja kingo zake na kusambaratisha shughuli za usafiri na kiuchumi katika eneo hili.

Daraja hilo lililoporomoka linaunganisha maeneo ya Kilgoris na Transmara Magharibi, Transmara Kusini, Narok, Migori, Isibania na Tanzania limewaacha wakazi na wasafiri wakihangaika kwa upatikanaji wa huduma muhimu.

Akizungumza na waandishi wa habari kwa niaba ya wahudumu wa bodaboda wa eneo hilo, mwenyekiti wa bodaboda eneo hilo Simon Nkanasa alisema kuwa hali hiyo imezua wasiwasi miongoni mwa wazazi waliokuwa wakijiandaa kuwapokea watoto wao kutoka Shuleni mwao kwa mapumziko ya likizo fupi.

Alibainisha kuwa kutokana na wasiwasi wa kiusalama, baadhi ya familia sasa zinafikiria kuwarejesha shule watoto wao.

Aliendelea kusema kuwa walikuwa wamefurahia kuwakaribisha watoto wao nyumbani, lakini kutokana na daraja kuporomoka, usalama wao sasa uko hatarini.

Aidha alisikitika kuwa njia ya pekee inayopatikana inapitia Kaunti ya Migori na ina urefu wa takriban kilomita 150 zaidi kuliko ile ya kawaida ya daraja la Mogor, hivyo basi kuongeza pakubwa gharama za usafiri kwa wakaazi na wafanyabiashara.

Nkanasa aliongeza kuwa wafanyabiashara pia wameathirika pakubwa, kwani harakati za biashara kati ya pande hizo mbili zimekwama kabisa. Alizitaka serikali zote mbili kulipa kipaumbele jambo hili la ujenzi wa daraja hilo ili kurejesha hali ya kawaida.

Mkaazi mwingine, Ezekiel Eboo, alieleza kusikitishwa ya kuwa hakuna ukarabati uliofanywa katika daraja hilo tangu lilipojengwa wakati wa ukoloni.

Eboo alionya kuwa hali hii iliyoshuhudiwa leo inaleta hatari kubwa kwa wagonjwa wanaohitaji matibabu ya haraka, kwani itakuwa vigumu mno kuwahamishia katika vituo vya afya vinginevyo. Pia alitabiri changamoto zaidi kwa wazazi wakati wa kipindi cha kuwarudisha wanafunzi shuleni baada ya likizo fupi katikati ya muhula wa kwanza.

Wakazi sasa wanatoa wito kwa serikali kuharakisha ujenzi wa daraja la Mogor, wakieleza kuwa Daraja hiyo ni kiungo muhimu kinachosaidia huduma katika sekta mbalimbali kama vile elimu, huduma za afya, biashara na shughuli zinginezo za muhimu katika maisha ya ya kila siku wakaazi wa maeneo husika.

Mwisho/Maendeleo/Mwangi/ Abuya

Maelezo ya picha

Aliyekuwa gavana wa Narok, Samuel Tunai ( aliyeelekeza mkono wake kwa daraja la Mogor) afika eneo la barabara ya Lologorian-Kilgoris ambapo daraja la Mogor liliporomoka hii leo na kukatiza shughuli nyingi muhimu ikiwemo ile ya usafiri baada ya mvua mkubwa kunya katika eneo hilo.