Narok, Ijumaa, Februari 27, 2026 KNA na Emily Kadzo

Watoto wanaoishi na ulemavu kuendelea kupokea huduma sawia – Kamishna

Wanafunzi wanaoishi na ulemavu katika Kaunti ya Narok wataendelea kupokea huduma za kiserikali sawa na wanafunzi wengine, huku yeyote anayeshikilia mila na tamaduni zilizopitwa na wakati zinazowabagua akionya kukabiliwa na hatua kali za kisheria.

Kauli hiyo ilitolewa na Kamishna wa Kaunti ya Narok, Kipkech Lotiatia, wakati wa hafla ya utoaji wa zaidi ya shilingi 500,000 na Baraza la Kitaifa la Watu Wanaoishi na Ulemavu (NCPWD) kusaidia elimu ya wanafunzi wanaoishi na ulemavu. Alisema ubaguzi ni dhana potovu inayowakosesha watoto hao fursa ya kufikia malengo yao maishani na kusisitiza kuwa serikali itaendelea kuwalinda.

Kamishna alieleza kuwa watoto wanaoishi na ulemavu wana haki sawa ya kupata elimu, ufadhili wa serikali na huduma nyingine za umma. Aliwahimiza wazazi na walezi kuhakikisha watoto wao wanasajiliwa na NCPWD ili kutambulika rasmi na kurahisishiwa upatikanaji wa msaada.

Mwenyekiti wa NCPWD eneo la Narok, Julius Ntaiya, alisema baraza hilo linaendelea kujizatiti kuhakikisha watoto wanaoishi na ulemavu wanapata elimu kama watoto wengine nchini. Alitoa wito kwa wazazi na walezi kushirikiana na serikali kwa kuwasajili watoto wao, akibainisha kuwa serikali imetenga rasilimali mahususi za kuwainua.

Wanufaika wa ufadhili huo walitoa shukrani wakisema msaada huo umefika kwa wakati muafaka na utawapunguzia mzigo wa kifedha huku ukibadilisha maisha yao.

Damaris Nailantei alisema ufadhili huo ulimwezesha kumlipia karo mtoto wake anayeishi na ulemavu, jambo ambalo limekuwa changamoto kubwa kutokana na ufinyu wa fedha.

Huko Narok Magharibi, Ole Moonka, anayeishi na ulemavu, alisema alipokea mashine ya kuosha magari kupitia NCPWD, hatua aliyosema imeongeza kwa kiasi kikubwa uhuru wake wa kiuchumi.

Aliongeza kuwa umiliki wa kadi ya NCPWD huruhusu watu wanaoishi na ulemavu kupata huduma za matibabu bila malipo, na kuwahimiza wenzake kujiandikisha ili waweze kupokea mawasiliano na huduma stahiki kwa wakati.

Hatua hizi zinaashiria juhudi za serikali za kuhakikisha watu wanaoishi na ulemavu wanashirikishwa kikamilifu katika shughuli za maendeleo na hawaachwi nyuma.

Mwisho/Maendeleo/Ngala/Githaiga

Maelezo ya picha

1000599424.jpg: Kaunti Kamishna wa Narok, Kipkech Lotiatia, akimkabidhi mwanafunzi anayeishi na ulemavu hundi ya karo ya shule katika afisi za NCPWD mjini Narok.

1000599425.jpg: Kaunti Kamishna wa Narok, Kipkech Lotiatia, akihutubia waliohudhuria hafla ya utoaji wa zaidi ya shilingi 500,000 za karo kwa watoto wanaoishi na ulemavu katika afisi za NCPWD mjini Narok.

Top of Form

Bottom of Form